Posted by : Unknown
Monday, 12 May 2014
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
Katika mikakati ya kupambana na ujangili nchini,
serikali imesaini mikataba minne ya makubaliano na tasisi za kimataifa
kwa ajili ya kutatua janga hilo.
Mikataba hiyo ilisainiwa juzi jijini Dar es Salaam kati ya serikali na
taasisi hizo ambazo ni UNDP, Benki ya Dunia, International Conservation
Caucus Foundation (ICCF), Global Environment Facility (GEF) na
makubaliano hayo yamejikita katika kuisaidia Tanzania kupambana na
ujangili.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa siku mbili kwa ajili ya
kujadili mkakati wa kupambana na ujangili, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
alisema mkakati wa kupambana na ujangili ni muhimu nchini.
Alisema Tanzania ina hifadhi 16 za mbuga za wanyama hivyo mkakati huo utasaidia kutatua tatizo la ujangili nchini.
Pinda alisema wanyama hao ni muhimu kwani bila wanyama hao pato la taifa
litashuka kwani serikali inaitegemea sekta hiyo katika kukuza uchumi wa
nchi.
Hata hivyo, alisema uwindaji wa wanyama hao umekuwa ni tatizo la muda mrefu nchini.
Aliongeza kuwa katika kupambana na ujangili huo serikali imewakamata majangili 2085 na kuwafungulia kesi.
"Pia tumeteketeza 1721 silaha ambazo zilikuwa zikitumika kuwindia
wanyama, tumejitahidi kushinda vita hiyo ila bado imekuwa ni changamoto
kwetu," alisema.