Dodoma. Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika imepita kwa kusuasua baada ya wabunge wanane kutishia na
kujaribu kuiondoa shilingi katika mshahara wa waziri.
Bajeti hiyo, ambayo ilisomwa na kupitishwa juzi,
ilikutana pia na kauli za kutaka Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Christopher Chizza ajiuzulu kwa madai kuwa ni mzigo na ameshindwa
kuiendesha wizara hiyo.
Ilibidi Chizza afanye kazi ya ziada kujieleza
baada ya mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage kutishia kuondoa
shilingi kutokana na tatizo la ugonjwa wa migomba, unaojulikana kama
mnyauko, kutotatuliwa.
“Nasikitika Serikali haikunielewa nilichosema kuwa
sasa Kagera kuna njaa. Haikunielewa kinachopaswa kufanyika kwa sababu
huu ni ugonjwa unatokana na mgusano,” alisema Mwijage, hoja iliungwa
mkono pia na mbunge wa Viti Maalumu, Benadeta Mshashu (CCM).
Kutokana na mabishano hayo, mwenyekiti wa Bunge,
Mussa Azzan Zungu alimtaka Waziri Chizza kukubali kupeleka chakula ili
shilingi yake ibaki akatumie na mkewe, jambo alilokubali.
Moto mwingine uliwashwa na mbunge wa Kasulu Mjini,
Moses Machali (NCCR-Mageuzi) aliyeondoa shilingi baada ya kushikilia
msimamo wake wa kutaka Serikali kukaa na wadau wa kilimo na kutafuta
njia ya kuondoa ubadhilifu katika pembejeo.
Uamuzi huo uliungwa mkono na mbunge wa Ubungo,
John Mnyika (Chadema) aliyesema kutengeneza mfumo ambao unamlazimisha
mkulima kuwa mwanachama wa chama cha ushirika ili apate mkopo, ni
kutengeneza chujio kwa wakulima katika suala la upatikanaji wa pembejeo.
Hata hivyo, Chizza alisema si wakulima wote waliokuwa wanapata ruzuku ya pembejeo katika utaratibu uliopita.
Hoja ya kuondoa shilingi ilishindikana kupita baada ya Zungu kuwahoji wabunge.
Wengine waliotishia kuondoa shilingi walikuwa ni
pamoja na mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany (CUF), na wa Bariadi
Mashariki John Cheyo, (UDP) ambaye alitaka kuruhusiwa kwa
wafanyabiashara wote kununua pamba.
Hoja ya Cheyo iliungwa mkono na mbunge wa Maswa
Magharibi, John Shibuda (Chadema) na mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi).
Hata hivyo, kulitokea malumbano mengine juu ya
muda watakaokutana wadau na Serikali baada ya Cheyo kutaka Chizza
kutamka siku hiyo bungeni.